Mwaka 2015 ulikuwa mwaka wa kihistoria katika
jamhuri ya muungano wa Tanzania, yaani kwa kuwa na matukio makubwa, tukio la
kwanza ni uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25,2015.Nauhita mwaka wa kihistoria
kutokana na kampeni za uchaguzi pamoja na uchaguzi wenye kuwa na tofauti na
miaka mingine iliyopita toka nchi ipate uhuru.Utofauti huo ni ushindani mkubwa
uliokuwepo kwa vyama vya siasa na jinsi kampeni zilivyoendeshwa.Uchaguzi kwa
Tanzania bara naweza kusema ulifanyika vizuri pamoja na kasoro za hapa na pale
kujitokeza lakini kwa Tanzania visiwani yaani Zanzibar zoezi la uchaguzi
halikumalizika vizuri kwa maana ya
matokeo ya uchaguzi kufutwa.
Uchaguzi huo ulifutwa kwa kile kinachodaiwa kuwa
uchaguzi ulikuwa na kasoro nyingi ambazo zilipelekea chombo chenye mamalaka
yaani tume ya uchaguzi Zanzibar( ZEC) kupitia mwenyekiti wake kutangaza kufutwa
kwa uchaguzi kwa sababu kuu niliyoileza hapo awali.Hali hiyo imepelekea kile
kinachoitwa mkwamo wa kisiasa( Political impasse).Mkwamo huo wa kisiasa umeibua
maswali mengi kwa watu mbalimbali na taasisi mbali mbali,kwa mujibu wa
waangalizi wa ndani na nje wanasema zoezi lilienda vizuri hakuna kasoro
zilizojitokeza kama inavyodaiwa na tume,wapo wengine wanauliza uhalali wa tume
kwa maana ya tume kuwa zinajitokezaje kasoro kubwa zinazopelekea mpaka matokeo
yote ya ya uchaguzi kufutwa, je tume haikuwa imejiandaa kuhakikisha zoezi
linafanyika kwa weredi? Na wengine wanadai kitendo cha mwenyekiti kufuta
matokeo bila kamati kukaa ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria
ilivyo/inavoelekeza.
Hatuwezi kupuuza wasiwasi wa watu hao walionao juu
ya kilichotokea Zanzibar.Kama wakaguzi
wa ndani na nje walijiridhisha na kuweza kutoa taarifa juu ya zoezi la uchaguzi
kwenda vizuri,kwa nini tume ya uchaguzi iliamua kufuta matokeo ya uchaguzi
huo?, je tume imeamua kufanya hivyo kwa maslahi ya nani?,mimi siamini kama
matokeo yote yanaweza kuwa na kasoro wakati kuna watu maalum walikuwepo wakisimamia
zoezi hilo kuhakikisha linafanyika vizuri. Kama tume imeamua kuchukua uamzi huo
kwa maslahi ya watu wachache au chama,itambue kufanya hivyo ni kinyume na
demokrasia na nikinyume na katiba,kama tuliamua kuwa nchi ya kidemokrasia na
kuruhusu mfumo wa vyama vingi basi hatuna budi kukubaliana na matokeo ya mfumo huo.
Afrika imekuwa na changamoto kubwa hasa linapokuja
suala la demokrasia na mfumo wa vyama vingi,vyama tawala vimekuwa vikitumia
nguvu dora kufunja sheria na kukiuka katiba hasa vinapoonekana kuelekea
kushindwa na vyama vya upinzani katika chaguzi,nafikiri hili ndilo limekuwa
likipelekea hata matokeo ya uchaguzi kufutwa au kuchelewa kutangazwa kwa baadhi
ya vituo vya uchaguzi.Nadhani vyama
tawala vinasahau kuwa wananchi ndiyo wenye nchi,hivyo wakiamua kuchagua chama
wanachokiona kwao ni sahihi hakuna
sababu ya kutumia nguvu dora na ukiukwaji wa katiba kwa kupindisha sheria na
kumweka mtu ambaye chama tawala kinamtaka,wananchi wameamua hivyo lazima
tuheshimu maamuzi yao.Kama wazanzibari wameamua kumchagua wanayemtaka basi
tuheshimu maamuzi yao na hiyo ndiyo demokrasia ya kweli.
Baada ya matokeo ya uchaguzi kufutwa ,tume hivi
karibuni ilitangaza tarehe ya uchaguzi kurudiwa yaani tarehe 20 Machi,2016.Sikuona
sababu ya msingi ya uchaguzi kurudiwa,huu mkwamo wa kisiasa ungeweza kutatuliwa
kwa mazungumzo ya pande mbili kufanyika yaani CCM na CUF.Nikinukuu maneno ya
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi hivi majuzi katika sherehe za maadhimisho ya
Chama cha Mapinduzi kutimiza miaka 39,”Alisema hakupenda uchaguzi urudiwe”.Nafikiri
hiyo ingekuwa fursa ya pande mbili
yaaani CCM na CUF kutanguliza maslahi ya
taifa na mazungumzo kufanyika na hatimaye kufikia muafaka na matokeo kutangazwa.Kurudia uchaguzi kwanza ni gharama na inaweza
kupelekea wazanzibari kutokwa na imani na tume ya uchaguzi na mwisho inaweza
kuleta uadui kwa vyama na serikali hasa kwa wananchi kuichukia serikali iliyopo
na kuona hakuna sababu ya wao kushiriki katika chaguzi mbalimbali kwa sababu
tume haiaminiki tena.
Mimi naamini, endapo Chama Cha Mapinduzi kikiamua kutanguliza
maslahi ya taifa mbele basi suluhu inaweza
kupatikana kwa urahisi,naamini mpaka
sasa Chama Cha wananchi CUF kimeonesha ukomavu kwa kutaka suluhu iwepo.Hivyo
fursa hiyo itumike vizuri kwa maslahi ya Zanzibar na Jamhuri ya muungano kwa
ujumla .
Chagulani,Shabiru
10/2/2016