7/16/2015

Je,Magufuli atatukomboa?



Je,  Magufuli atatukomboa?
Hivi karibuni Chama Cha Mapinduzi kilikua na vikao ambavyo vilipelekea kumpitisha John Pombe Magufuli kama Mgombea Urais kupitia CCM  katika uchaguzi unaotegemewa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.  
Kwanza, nachukua fursa hii kumpongeza kwa kupitishwa na kuwa mgombea wa CCM  katika  uchaguzi utakao fanyika mwezi Oktoba,haikuwa kazi  rahisi kufikia uamzi huo lakini kupitia vikao vilivyofanyika kwa muda mrefu hatimaye aliweza kupitishwa.
Leo katika makala haya tunaangalia kama mgombea huyo anaweza kuwa Mwarobaini kwa matatizo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
John Pombe Magufuli  ni mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa, hasa ukizingatia kuwa amekuwa waziri kuanzia awamu ya tatu mpaka awamu ya nne, pia anasikifa kwa kuwa mchapakazi na mtu mwenye maamuzi ya haraka  katika kutafuta ufumbuzi wa jambo lolote.Yote hayo yamedhihirika katika wizara mbalimbali alizozipitia, hivyo ana uzoefu wa masuala mbalimbali katika wizara mbalimbali na utendaji  kwa ujumla.
Kwa mtazamo huu nilioeleza hapo juu, ndugu Magufuli anaonekana kama malaika au mkombozi machoni mwa watu wengi, mtazamo huo unaweza kufanana  na ule wa  watu waliokuwa nao mwaka 2005 kipindi Jakaya Kikwete alipopitishwa na kuanza kufanya kampeini sehemu mbalimbali za nchi, wengi walionekana kummunga mkono wakitegemea kuwa ndiye mkombozi wao, hivyo waliimunga mkono na kuweza kushinda  uchaguzi kwa asilimia kubwa. Hivyo hali hiyo inaweza kujirudia tena  mwaka huu katika uchaguzi.
Ukisoma ibara ya 8 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ya mwaka  1977  inasema hivi katika vifungu a,b na c ( a)”.Wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na serikali itapata madaraka na mamalaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii” ( b)”.lengo kuu la serikali  litakuwa  ni ustawi wa wananchi” ( c)Serikali itawajibika kwa wananchi. Kwa nukuu ya vifungu hivyo hapo juu, tunaweza kupima kama serikali ya awamu ya nne iliweza kutimiza wajibu wake kikatiba kwa kuhakikisha ustawi wa wananchi wake, kwanza katika; afya, maji, elimu, umeme na miundombinu. Nafikiri wewe  msomaji wa makali hii unaweza  kujua hali halisi ilivyo katika sekta ya afya ambapo ni rahisi kwenda hospitali ukaambiwa hakuna dawa wala vifaa tiba hali ambayo imekuwa ikiipelekea vifo hasa  kwa mama wajawazito na watoto,  pili sote tunafahamu kuwa  maji bado ni tatizo mijini na vijijini, elimu nayo inayotolewa  sio bora na inafahamika uwepo wa changamoto mablimbali kt sekta ya elimu. Changamoto hizo tumekumbana nazo ktk awamu ya nne kwa kipindi cha miaka kumi chini ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi kilichotoa ahadi ya “Maisha Bora kwa kila Mtanzania.”
Naamini Magufuli haya yote anayajua vizuri maana amekuwa mbunge kwa kipindi cha miaka ishirini, pia ni miongoni mwa wabunge  walioshuhudia  matukio ya ufisadi toka awamu ya tatu  mpaka ya nne, lkn alishiriki katika bunge maalum la katiba na kuweza kupitisha katiba pendekezwa  ya CCM na kupuuza ile iliyokuwa imependekezwa na wananchi.Je mnawezaje kumpa ridhaa mtu huyu ambaye anaamini katika maslahi ya chama kwanza kuliko taifa?.
Nafikiri ifike pahala watanzania  tuache ugonjwa wa kusahau tuliyoyapitia ktk awamu ya nne.Tutakuwa tunajidanganya kutegemea  ukombozi wa kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya taifa kupitia Chama Cha  Mapinduzi, tumeshuhudia mengi bungeni ambapo wabunge walionekana wapo tayari kutetea uovu  kwa vijembe na kejeli kwa maslahi ya chama, pili wamekuwa tayari kufanyanya lolote hata kama linakiuka sheria kanuni na utaratibu ili kutimiza maslahi ya chama bila kujali lolote linazoweza kujitokeza na kuathiri uchumi wa taifa,hii inaweza kudhihirishwa na utetezi wa wabunge wa CCM ktk skendo ya escrow,pia tumeshuhudia miswada ya gesi na mafuta ikipitishwa akidi bila kutia na wadau mbali mbali bila kushirikishwa na miswada kutojadiliwa kwa kina.
Kwa kuhitimisha, Chama Cha Mapinduzi hakipo tayari kumkoboa mwananchi na kuhakikisha ustawi wake na Taifa  kwa ujumla.Miaka kumi inayoelekea ukomo wake Oktoba inaweza kusaidia katika kufanya tathimini.Tuna mengi yakujifunza kwa kufanya maamuzi kama wenzetu Kenya na Nigeria walivyofanya.
Kura yako ni silaha yako, itumie vizuri
Chagulani, Shabie